Kenya Imekuwa Bora Kutokana na Walibora

Prof.Ken Walibora. PICHA: Chuo Kikuu cha Riara

Huku taifa zima likiendelea kuomboleza kifo cha ghafla cha gwiji wa Kiswahili Prof. Ken Walibora, kipindi hiki cha maombolezi pia ni cha kutafakari kuhusu mchango
wake mkubwa katika kuikuza lugha ya Kiswahili nchini.

Ni wazi kuwa wengi wameelezea hisia za walivyomfahamu Walibora, walivyotagusana naye na jitimiai zao kufuatia  kifo chake.

Binafsi nilimfahamu Walibora mara ya kwanza nikiwa shule ya msingi miaka ya 90. Baadaye nikiingia shule ya upili, tayari riwaya yake ya Siku Njema ilikuwa ikitahiniwa kiwango cha shule ya upili kama kitabu cha lazima.

Siku Njema ndicho kitabu kilichoikonga ari yangu ya kuifahamu lugha ya Kiswahili. Nilikisoma kitabu hicho kwa mara ya kwanza nikiwa kidato cha kwanza mwaka wa 2000.

Kikubwa zaidi, mhusika mkuu wa riwaya hiyo, Msanifu Kombo, ambaye baadaye alifahamika kama Kongowea Mswahili, alikuwa kielelezo chema cha ukakamavu tunaostahili kuwa nao katika maisha.

Tulijifunza kutoka kwa Kongowea Mswahili umuhimu wa maadili mema na kutokata tamaa maishani. Kwamba ni jambo bora  kujikaza kisabuni kuafikia maazimio yetu licha ya pandashuka za maisha.

Safari ya kuitafuta asili yake, kutoka Tanga nchini Tanzania, hadi Mombasa na hatimaye Kitale nchini Kenya, ni hamasa kubwa kwa kila binadamu anayeifuata ndo yake maishani.

Maudhui muhimu ya riwaya hiyo ilikuwa ni mabadiliko. Kauli ikiwa, hakuna kinachodumu duniani ila mabadiliko. Wahusika wote wakuu kwenye riwaya hiyo walipitia changamoto mbalimbali, lakini mwishowe, walifungua kurasa mpya maishani mwao. Hata Amina aliyekuwa kahaba, aliyageuza maisha yake.

Kwa wengi wetu enzi hizo ,hatukufahamu kuwa Ken Walibora alikuwa Mkenya kutokana na kiwango cha lugha alichoitumia katika riwaya ya Siku Njema, hususan, mazingira walimoishi wengi wa wahusika wake.

Katika uhai wake na mauti yake, taifa letu limebahatika pakubwa kutokana na mchango wake. Pengine ni jukumu letu tuliobaki kuendeleza kazi nzuri aliyoianzisha marehemu Walibora. Kila mmoja wetu anaweza kufanya kilicho ndani ya  uwezo wake, kuchangia ukuaji wa lugha ya Kiswahili, kupitia kujifunza and kuizungumza kila mara.

Kiswahili lugha ya taifa

Katiba yetu imeikweza Kiswahili kwenye hadhi ya juu kama lugha ya kitaifa. Akiwa hai, Prof. Walibora alitaka sana lugha ya Kiswahili ipewe uzito sawa na ule wa lugha ya Kiingereza hususan katika taasisi za elimu.

Alihoji kuwa taasisi nyingi za elimu nchini hasa shule za msingi na upili zinaegemea pakubwa uzungumzaji wa lugha ya Kiingereza kama kigezo cha ustaarabu na kwa kufanya hivyo, kuilemeza lugha ya Kiswahili .

 ‘‘Hakuna nchi duniani ambayo inachagua lugha ya watu wengine, na kusema hiyo ndiyo lugha na kuikana lugha yao wenyewe. Lakini sisi Waafrika katika hali zetu za kasumba ya ukoloni tunafikiria kwamba tutakuwa waliostaaribika kama tutazungumza Kiingerea katika maeneo ya shule na watoto wasiruhusiwe kuzungumza Kiswahili.Hayo yanakwenda kinyume, mwanzo na katiba. Katiba ya Kenya inasema kwamba Kiswahii ni lugha ya Kitaifa. Hilo ni jambo la kimsingi,’’ alisema Walibora mwaka wa 2018.

Hiyo ndiyo iliyokuwa falsafa yake Walibora. Kama mwanazuo, alidhihirisha hilo kupitia usomi wake na utafiti uliochangia ukwasi mkubwa katika lugha ya Kiswahili. Mbali na hiyo, vitabu vipatavyo 40 alivyochapisha vitakasalia urathi mkubwa kwa taifa la Kenya.

Kifo cha Walibora kimetupokonya johari adimu na thamini. Alikuwa kwetu maridhia wala badala yake hatutampata mwingine.

Kenya imekuwa bora kwa kuwa Walibora alikuwa mmoja wetu.

Ujumbe wa mhariri: Kwa kuwa uko hapa, tungependa kufahamu mtazamo wako kuhusu makala hii. Unaweza kuipenda, kushiriki na hata kutoa maoni yako!


 

Advertisement

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.